Mwili huo ambao uliwasili saa 1:05 jioni kwa ndege
ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini(SAA), ulipokewa na wanafamilia
akiwamo mke wake pamoja na watoto ambao walikuwa wamevalia suti nyeusi,
Viongozi mbalimbali wa kitaifa walifika uwanjani
hapo kuupokea mwili wa Dk Mvungi, akiwamo Waziri wa Uchukuzi, Dk
Harrison Mwakyembe, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi
na Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Angela Kariuki.
Pia wajumbe wote wa Tume ya Katiba walikuwapo
uwanjani hapo wakiongozwa na Mwenyekiti, Jaji Joseph Warioba pamoja na
Mwenyekiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen
Kijo Bisimba.
Akizungumza na gazeti hili uwanjani hapo, mtoto wa
kwanza wa marehemu Dk Mvungi, Dk Natujwa Mvungi alisema, pengo
aliloliacha baba yao ni kubwa kwa familia nzima, kwani licha ya kuwa
baba, Dk Mvungi alikuwa mwalimu, kiongozi na kocha wa maisha yao.
“Hatuwezi kumlaumu Mungu kuwa baba amefariki
tunachoshukuru ni kuwa alituandaa kuyakabili maisha kimasomo na
kibusara. Kwa hivyo tunamwombea apumzike salama,” alisema Dk Natujwa.
Dk Natujwa alisema jambo ambalo analifurahia kwa
baba yake ni kuwa aliifanya kazi yake ambayo alikuwa akiitamani kwa muda
mrefu ya kushiriki katika mchakato wa kuunda Katiba Mpya.
“Ingawa hakuimaliza safari yote ya kuunda Katiba
Mpya, lakini ameshiriki na amefanya kazi ambayo kila siku katika maisha
yake alikuwa akiitamani. Alitamani sana kuifanyia marekebisho Katiba ya
Tanzania,” alisema.
Dk Natujwa alisema baba yake aliipenda nchi yake
na aliweka mbele utaifa kwanza kabla ya mambo yote, kwani siku zote
katika maisha yake alitamani Mtanzania amiliki rasilimali za taifa.
Mratibu wa Tume ya Katiba, Abdallah Witawi alisema
tume hiyo imepoteza nguzo muhimu ambayo hakuna mtu mwingine anayeweza
kuiziba kutokana na umahiri, elimu na uhodari aliokuwa nao Dk Mvungi.
Witawi alisema Dk Mvungi alikuwa ni mwadilifu,
mchapakazi na mzalendo ambaye alikuwa na uwezo wa kutumia chochote na
wakati wowote ili kushiriki katika kuijenga Tanzania,
“Alikuwa ana ndoto ya kuibadilisha katiba ili tu
Mtanzania anufaike na kile anachokifanyia kazi, lakini kikubwa zaidi
kwake ni kuwa alikuwa na ushirikiano mzuri na wajumbe wote. Alikuwa
anasikiliza ushauri wa mtu yeyote bila kujali elimu, umri au chama gani
cha siasa,” alisema
No comments:
Post a Comment