Dar es Salaam. Siku chache baada ya kukamatwa kwa tuhuma za
kutumia sare za polisi bila kibali katika video ya wimbo ‘Salamu Zao’,
na kisha kufikishwa katika Kituo cha Polisi Urafiki Manzese Jijini Dar
es Salaam, rapa wa muziki wa kizazi kipya, Ney Wa Mitego amesimulia
mkasa mzima na kusisitiza kuwa wabaya wake ndiyo waliycheza mchezo huo.
Akizungumza na Mwananchi, rapa huyo alisema sare
hizo za polisi zilishonwa kwa ajili ya kazi hiyo na wala hazikuwa sare
halisi za kipolisi.
“Mavazi haya ya kipolisi yalikuwa rasmi kwa ajili
ya kutengeneza video ya Salamu Zao na hayakuwa halisi, ila nilishangaa
pale nilipokamatwa na watu wasiojulikana jumamosi ya wiki iliyopita
wakati tukitengeneza video, wakidai kwamba wao ni askari.Walinichukua
hadi kituo cha urafiki, pale niliwekwa sero kwa kipindi cha dakika 20
hivi, baada ya kutoa maelezo ya kutosha niliachiwa”.
Baada ya kuachiwa, alirudi na kukamilisha kazi yake ambayo ameweka wazi kuwa itakuwa hewani wiki hii.
“Video ya Salamu Zao itaachiwa hewani Ijumaa ya
wiki hii, hivyo watarajie kitu kipya na adimu kuonekana,” alisema Nay na
kuongeza “Sijajua bado ni nani aliyenichomea lakini naahidi kuwa
itaendelea kula kwao wale wote wanaonichukia na kamwe siwezi kuacha
kuusema ukweli.”
Uongozi wa kituo cha Polisi Urafiki jijini Dar es
Salaam ulithibitisha kumtia mbaroni msanii huyo kwa kukutwa akitumia
sare zinazofanana na mavazi ya polisi kinyume cha sheria. Ofisi mmoja wa
polisi ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini anasema waliamua
kumuachia kwa vile waliridhika na maelezo yake.
No comments:
Post a Comment