UMEME KUADIMIKA KWA TAKRIBAN SIKU 11 NCHINI: Wateja katika mikoa inayopata umeme kwenye gridi ya Taifa wanatarajiwa kupata adha ya upungufu wa umeme kwa siku 11 kuanzia leo, kutokana na upungufu wa gesi kutoka katika Kisiwa cha Songosongo kilichopo wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi..........
WATEJA katika mikoa inayopata umeme
kwenye gridi ya Taifa wanatarajiwa kupata adha ya upungufu wa umeme kwa
siku 11 kuanzia leo, kutokana na upungufu wa gesi kutoka katika Kisiwa
cha Songosongo kilichopo wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi.
Hali hiyo imetajwa inatokana na kuwapo
kwa matengenezo ya kiufundi kwenye visima vya gesi unaofanywa na Kampuni
ya Pan African Energy Tanzania Limited (PAT).
Meneja Uhusiano wa TANESCO, Badra Masoud
aliyasema hayo Dar es Salaam jana, akisema upungufu huo utatokea kati
ya Novemba 16 hadi Novemba 26, mwaka huu na itahusisha maeneo yaliyopo
katika mikoa iliyounganishwa katika gridi ya Taifa.
“Tumepata barua kutoka kwa kampuni ya
Pan African inayotuuzia gesi, wakisema inafanya matengenezo hayo
kuboresha upatikanaji wa gesi ya kutosha kwenye visima hivyo. Uongozi
unaomba radhi kwa usumbufu utakaojitokeza kwa baadhi ya maeneo
yatakayokuwa yakikosa umeme,” alisema.
Kwa mujibu wa Masoud, kutokana na
matengenezo hayo mikoa iliyounganishwa katika gridi ya Taifa itaathirika
kwa kukosa umeme kwa baadhi ya maeneo na kwa nyakati tofauti na
kuongeza huduma ya umeme ni muhimu kwa kila Mtanzania kwa ajili ya
kujiinua kiuchumi na kipato, lakini matengenezo hayo ni muhimu kwani
itaboresha upatikanaji wa gesi kwa ufanisi zaidi.
Aliitaja mikoa na maeneo yatakayokumbwa
na upungufu wa umeme kuwa ni Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro,
Arusha, Dodoma, Morogoro, Singida, Mwanza, Mara, Mbeya, Iringa, Tabora,
Shinyanga, Manyara na Zanzibar.
Masoud alisema gesi imekuwa ikiwawezesha
kutoa Megawati 100 katika kituo cha Ubungo 1, Megawati 100 katika kituo
cha Ubungo 2, kituo cha Tegeta Megawati 45 wakati Kampuni ya Songas
imekuwa ikitoa Megawati 182 na kuongeza kutokana na matengenezo hayo
kutakuwa na upungufu wa Megawati kati ya 150 na 200 na kwamba uzalishaji
wa umeme kutumia mafuta na maji utaendelea.
Alisisitiza kuwa upungufu huo wa umeme
sio mgawo ila ni kupitisha matengenezo ya kiufundi ya Kampuni ya Pan
African ambayo alidai kuwa ilishaiomba Tanesco miezi miwili iliyopita
ikitaka kufanya matengenezo hayo ambayo hayaepukiki na yenye lengo la
kuleta ufanisi zaidi.
Masoud alitoa wito kwa wananchi kuwa
wavumilivu siku hizo 11 wakati matengenezo yakifanyika na kuwa lengo ni
kuboresha upatikanaji wa gesi ya kutosha kwa ajili ya kuzalisha umeme wa
kutosha na kutoa huduma inayoridhisha ya nishati ya umeme kwa wateja
wake
No comments:
Post a Comment