Makubaliano ya amani kati ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo na waasi wa M23 ,huenda yakatiwa saini Jumatatu ijayo mjini Kampala, Uganda,kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uganda.
Mkuu wa kijeshi wa waasi wa M23, Sultani Makenga
Makubaliano hayo ndiyo yanayotarajiwa kutaja juu ya hatima ya wapiganaji wa kundi hilo la waasi na hasa wale waliokimbilia Uganda hivi karibuni. Miongoni mwao anakutikana pia mkuu wa kijeshi wa M23, Sultani Makenga.
"Makubaliano yako tayari, tunasubiri pande zote zirejee Kampala Jumatatu ili kutia saini," amesema msemaji wa serikali ya Uganda, Ofwono Opondo, na kufafanua wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, na wale wa Umoja wa Afrika wanatarajiwa pia kufika Kampala.
Msemaji huyo wa serikali ya Uganda amesema makubaliano ya amani yatakayotiwa saini Jumatatu ijayo ndiyo yatakayoamua kuhusu hatima ya wapiganaji wa M23 wanaokutikana nchini Uganda.
Ameongeza kusema miongoni mwa wanamgambo hao kuna wale ambao wamewekewa vikwazo na Umoja wa mataifa na Marekani na kuna wengine ambao wanataka kujumuishwa katika jeshi la Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo na wengineo ambao wangependelea kurejea nyumbani tu.
Msemaji wa wizara ya ulinzi na jeshi la Uganda, kanali Paddy Ankunda, amesema wanamgambo waliokimbilia Uganda si wafungwa na kwamba Uganda haitowakabidhi kwa serikali ya Kinshasa kabla ya makubaliano ya amani kutiwa saini.
Kongo itasaini makubaliano ya amani
Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, Lambert Mende, hakupatikana hadi leo mchana kutoa maoni yake. Hata hivyo alikwishatamka mapema wiki hii kwamba serikali yake imedhamiria kukamilisha ipasavyo utaratibu wa amani wa Kampala. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, Raymond Tshibanda, akiwa ziarani mjini Paris, Ufaransa, amethibitisha serikali yake itatia saini makubaliano ya amani ya Kampala Jumatatu ijayo.
Ikipata nguvu kutokana na ushindi wake kijeshi, serikali ya mjini Kinshasa inapinga kuwasamehe wakuu 80 wa M23 wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu wa vita na mengineyo, lakini inapanga kuwasamehe waasi wote wale watakaoahidi kutobeba tena silaha dhidi ya serikali.
Marais Kagame (kushoto) wa Rwanda, Museveni (kati) wa Uganda na Kabila wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo walipokutana November 12 mwaka 2012 mjini Goma
No comments:
Post a Comment